UHURU HATALEGEZA
Haya ni yangu maoni, wala sijapigwa “jeki”
Tarehe sita ya Juni, tungojao mahuluki
Vile nimetathmini, tutabakia kusaki
Uhuru hatalegeza, kutoa lokdauni
Mapema nawaeleza, nyote jitayarisheni
Yale mnayoyawaza, kando yote yawekeni
Henda nyembe mkameza, msidhani ni utani
Uhuru hatalegeza, kutoa ‘lokdauni’
Zilizowekwa sheria, kishogo hazitapewa
Wale mnaodhania, jioni mwende kulewa
Bure yenu nawambia, kafiu haitatolewa
Uhuru hatalegeza, kutoa ‘lokdauni’
Kama tulivyoambiwa, tutavaa barakoi
Sabuni itatumiwa, pamwe na masafi mai
Sote mikono kunawa, lodi na mlala hoi
Uhuru hatalegeza, kutoa lokdauni
Usinigwiie rungu, na kunipiga mateke
Haya ni mawazo yangu, huenda yasifanyike
Bora ni kuomba Mungu, janga hili litutoke
Uhuru hatalegeza, kutoa lokdauni